Serikali kumulika kodi mashirika yasiyo ya kiserikali

0
39

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema Serikali inaandaa kitini ambacho kitatoa mwongozo wa jinsi mashirika yasiyo ya kiserikali yanayofanya kazi kwa hisani yatakavyonufaika na misamaha ya kodi iliyopo kwa mujibu wa sheria.

Rais Samia ameyasema hayo leo Septemba 30, 2021 jijini Dodoma akizungumza katika mkutano mkuu wa Baraza la Taifa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (Nacongo) uliozikutanisha asasi hizo zinazofanya kazi nchini.

“Tunafahamu zipo changamoto kwenye mifumo yetu ya kodi na pia kuna baadhi ya taasisi zinastahili kupata misamaha ya kodi. Tumeanza kufanyia kazi yote hayo. Tumeandaa kitini kitakachoeleza namna mashirika yasiyo ya serikali, yanayofanya kazi kwa hisani zikakavyonufaika na misamaha ya kodi,” amesema Rais Samia.

Kauli hiyo ya Rais Samia imetokana na ombi lililotolewa na Mwenyekiti wa Nacongo, Dk Lilian Badi wakati na kueleza changamoto mbalimbali zinazoyakabili mashirika yasiyo ya serikali ikiwemo upatikanaji wa misamaha ya kodi , upatikanaji na uhuishaji wa vibali vya ukaazi kwa raia wasio Watanzania.

Mbali na hilo, Rais Samia ametumia jukwaa hilo kuyataka mashirika hayo kufanya kazi kwa kuzingatia maadili, tamaduni na mila za Kitanzania, kupunguza utegemezi wa kifedha kutoka kwa wahisani, kuhakikisha malengo yao yanalandana na yale ya serikali na kuhamasisha wananchi kuchanja na kiushiriki sensa ya watu na makazi mwaka 2022.