Serikali kuongeza fursa za mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu

0
25

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema Serikali itaongeza fursa za mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kutoka 223,201 hadi 252,245 ili kuwezesha na kuimarisha huduma ya utoaji na upatikanaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu wenye sifa na uhitaji

Ameyasema hayo Bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025.

“Serikali itatoa mikopo kwa wanafunzi 84,500 wa mwaka wa kwanza ambapo shahada ya kwanza 80,000, shahada za juu 2,000, wanaosoma nje ya nchi 500 na Samia Scholarship 2,000, pia itatoa mikopo kwa wanafunzi 157,745 wanaoendelea na masomo,” ameeleza Prof. Mkenda.

Ameongeza kuwa Serikali pia itatoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi 40 wenye ufaulu wa juu kwenye masomo ya sayansi hususan wanafunzi wa kike waliohitimu mtihani wa Kidato cha Sita na shahada ya awali kupitia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, pamoja na kutoa ufadhili kwa ajili ya shahada za juu ikiwemo eneo la fani ya mionzi na nyuklia.

Aidha, Prof. Mkenda amesema Wizara yake imefanikiwa kutekeleza vipaumbele vitano katika mwaka wa fedha 2023/24 ambavyo ni pamoja kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa mafunzo ya amali kwa sekondari na vyuo vya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, kuwezesha Ongezeko la fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya msingi, sekondari na ualimu.

Vipaumbele vingine ni kuongeza fursa na kuimarisha ubora wa elimu ya juu na kuimarisha uwezo wa nchi katika tafiti, matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu ili kuchochea ujenzi wa uchumi wa viwanda.

Send this to a friend