Serikali: Kupanda kwa bei ya nyama ni fursa kwa wafugaji

0
25

Serikali imesema malalamiko yaliyojitokeza hivi karibuni ya kupanda kwa bei ya nyama nchini yanaashiria ukuaji wa sekta hiyo ambapo wafugaji wameshauriwa kuwa huu ni muda mzuri kwa wao kuvuna na kuuza mifugo yao.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amebainisha hayo leo jijini Dodoma mbele ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji wakati wa uwasilishaji wa taarifa ya utendaji kazi wa Bodi ya Nyama nchini mbele ya kamati hiyo.

Ulega amesema kipindi cha nyuma wafugaji walikuwa wakilalamika kutopata masoko ya mifugo yao ila katika kipindi cha sasa uhitaji wa mifugo katika viwanda vya kuchakata nyama nchini umekuwa mkubwa pamoja na hitaji la nyama katika soko la ndani.

“Sekta ambayo ulikuwa hauwezi kuisikia inasemwa, lakini leo inakuwa mjadala hivyo ni wakati mzuri sana kwa wafugaji kuvuna na kuuza mifugo yao,” amesema Ulega

Amesema serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imetengeneza uhitaji wa nyama baada ya kufungua biashara ya kuuza nyama nje ya nchi hivyo uhitaji wa mifugo kwenye viwanda vya kuchakata hapa nchini umeongezeka.

Kwa upande wake Msajili wa Bodi ya Nyama nchini Dkt. Daniel Mushi ameiambia kamati hiyo kuwa uhaba wa nyama uliojitokeza hivi karibuni na kusababisha bei ya nyama kupanda ni fursa ya kufuga kibiashara na kunenepesha mifugo hiyo.