Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba amesema lazima matumizi ya Serikali na matumizi ya watumishi wa umma yaakisi ugumu wa maisha ya wananchi kufuatia athari zilizosababishwa na majanga ya UVIkO-19.
Amesema hayo leo bungeni jijini Dodoma wakati akisoma hotuba ya bajeti kuu ya Serikali kwa mwaka 2022/2023 na kubainisha kuwa Serikali imepanga kuchukua hatua za muda mfupi na muda mrefu ili fedha zitakazopatikana ziweze kufanya mambo muhimu nchini.
Hatua za muda mfupi zilizotajwa ni pamoja na kupunguza safari za ndani na nje, kukata fedha za ununuzi usio wa lazima, kupunguza ukubwa wa wawakilishi kwenye mikutano ya ndani na nje, na kupima mafuta ya magari ya Serikali kila mwezi kufuatana na shughuli za lazima. Utaratibu huo umetajwa kutumika kwa wabunge pia.
Aidha, katika hotuba yake Mwigulu amesema Serikali inapendekeza kufuta ada ya kidato cha tano na kidato cha sita ili kupunguza gharama zinazowakabili wanafunzi.
“Ili kuwapunguzia gharama watoto hao (wanafunzi wa kidato cha tano na sita) kama Mheshimiwa Rais alivyonielekeza baada ya kuguswa sana na shida wanazozipata, napendekeza kufuta ada ya kidato cha tano na sita. Kwa hatua hiyo elimu bila ada itakuwa kuanzia shule ya msingi mpaka kidato cha sita” amesema Mwigulu Nchemba.