Serikali kushirikiana na shule binafsi kuboresha sekta ya elimu

0
63

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi, hususan shule binafsi ili kuboresha sekta ya elimu nchini.

Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Chama cha Wamiliki wa Shule Binafsi Tanzania (TAPIE) mkoani Dar es salaam, amesema Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu haiwezi kuacha wadau wa elimu wakilalamika kwani uwepo wao unaisaidia Serikali.

“Nataka niwahakikishie kuwa Serikali imeendelea kukutana na TAPIE mara kwa mara, na hapa namwelekeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama kuratibu mkutano wa pamoja kati ya TAPIE na Wizara za Ardhi, Fedha, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ili kujadiliana kwa pamoja na kupata suhulu ya changamoto zinazowakabili,” amesema.

Aidha, Dkt. Biteko amewaasa TAPIE kuzingatia masharti yaliyoainishwa katika barua na vyeti vya usajili wa asasi zao, kwa kuwa kuna baadhi hukiuka masharti hivyo kusababisha migongano isiyo ya lazima na mamlaka zilizokasimiwa kusimamia sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya uendeshaji wa asasi za elimu nchini.

Naye, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amezipongeza shule binafsi kwa kufanya uwekezaji mkubwa ambao sasa unavutia baadhi wanafunzi kutoka nchi zingine kuja kusoma hapa nchini.

Send this to a friend