Serikali kutoa mikopo ya kujenga vituo vya mafuta vijijini
Katika siku ya tano ya ziara ya Waziri wa Nishati, January Makamba ya kijiji kwa kijiji, imemfikisha Kata ya Buselesele Jimbo la Chato na kuzungumza na wananchi wa Jimbo hilo pamoja na wa wananchi wa Jimbo la Busanda.
Moja kati ya vitu alivyozungumza Waziri Makamba ni suala la mafuta safi nchini, waziri amesema kwa sasa Serikali imepunguza masharti ya kujenga vituo vya mafuta, pia inahakikisha mafuta safi yanapatikana nchi nzima ili kuachana na mafuta ya kwenye vidumu.
Kwa upande mwingine amewataka watu wenye uwezo wa kujenga vituo vya mafuta vijijini wafike wizarani kwa ajili ya kupatiwa maelekezo.
“Kwa sasa tunakopesha pesa kwa yeyote anayetaka kujenga kituo cha mafuta kijijini, pesa hizi zipo na masharti ya kujenga vituo hivi yamelegezwa. Kwa sasa ukiwa na milioni 40 unajenga kituo. Watu waje wakope hizi pesa, tumetenga bilioni 2 kwa ajili ya watu kukopeshwa,” amesema Waziri Makamba.
Ziara ya Waziri Makamba kwa sasa imefika mkoani Kagera, mara baada ya kupita mkoa wa Mara, Simiyu, Mwanza na Geita.