Serikali kuwachukulia hatua wote waliohusika tukio la watu wa jinsia moja kuvishana pete
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale imesema inalaani tukio lililosambaa kwenye mitandao y kijamii likiwaonyesha watu wa jinsia moja wakivishana pete katika eneo la fukwe ya hoteli ya The Loop iliyopo Jambiani, Wilaya ya Kusini, Mkoa wa Kusini Unguja.
Kamisheni ya Utalii Zanzibar imesema kitendo hicho kilichotokea ni ukiukwaji wa moja kwa moja wa sheria mbalimbali za Zanzibar ikiwemo sheria ya utalii ya Zanzibar namba 6 ya mwaka 2009, kifungu 27 (2), inayolazimisha kila mradi wa utalii kuhifadhi na kuzingatia maadili na utamaduni wa Kizanzibari.
Aidha, Serikali imesema kwa sasa vyombo husika vya Serikali vinaendelea na uchunguzi na hatua stahiki zitachukuliwa kwa wote walioandaa, waliosimamia na waliohusika na tukio hilo.
Imeongeza kuwa imewahimiza wawekezaji, wadau na wageni kutoshiriki kitendo chochote ambacho kinaweza kusababisha mmomonyoko wa maadili, silka au kuvuruga amani katika jamii, na kuwasihi wananchi kuwa watulivu wakati vyombo husika vikiendelea kuchukua hatua.