Serikali kuwawajibisha wazazi wenye watoto wa mitaani

0
40

Waziri wa  wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amesema kuwa serikali inatarajia kuja na oparesheni maalum ya kuwaondoa watoto wote walioko mitaani.

Akizungumza na waandishi wa habari Kigamboni jijini Dar es Salaam katika ziara yake ya kikazi, Waziri Gwajima amesema kuwa utekelezaji wa mkakati huo tayari umeanza kufanyiwa tathmini, ambapo watoto hao watapelekwa shuleni, na kwa wale waliojiingiza kwenye uvutaji wa dawa za kulevya watapatiwa tiba.

Aidha, ameongeza kuwa serikali itafanya tathmini kwa mujibu wa sheria kwa kuangalia sababu zilizowafanya watoto wawe katika mazingira hatarishi, ambapo sheria hiyo itakwenda kuwawajibisha wazazi wasiotekeleza majukumu yao. 

“Kuna watoto wako mitaani kutokana na wazazi wao kutokuwajibika, tutakwenda kuchambua sababu, tuangalie wamekuja kwa sababu ya nini. Wasifikiri serikali itachukua tu watoto, ili ni suala la pamoja,” amesisitiza Waziri Gwajima.

Ametoa wito kwa wazazi ambao wanajua watoto wao wapo mitaani kuhakikisha wanawachukua badala ya kusubiri kuwajibishwa kwa mujibu wa sharia. Pia, amewataka wazazi na walezi kutumia shule za programu maalum za malezi kwa watoto chini ya miaka mitano ili kuwasaidia kuwa na malezi na elimu chanya.

Send this to a friend