Serikali kuwawezesha vijana wabunifu (startups na techhubs)
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema kuwa serikali inatambua uwepo wa vijana wajasiriamali na wabunifu walioanzisha kampuni mbalimbali zikiwemo za teknolojia na kwamba wataungwa mkono ili kuweza kukua zaidi.
Rais ametoa ahadi hiyo akizungumza na wananchi wilayani Chato mkoani Geita katika maadhimisho ya Kilele cha Mbio za Mwenge kilicheokwenda sambamba na Kumbukizi ya Miaka 22 ya Kifo cha Hayati Mwl. Julius Nyerere na Wiki ya Vijana.
“Serikali inatambua vijana wengi wajasiriamali na wabunifu wameanzisha ‘startups’ na ‘techhubs,’ na hivyo serikali itaangalia namana ya kuwawezesha zaidi ili muweze kukua na kuwa wabunifu wa kimataifa,” amesema Rais Samia.
Aidha ameongeza kwamba Tanzania inakusudia kujenga chuo kikubwa sana cha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ambacho kitakuwa kikubwa zaidi Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Hata hivyo ameungana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuwatahadhari vijana ambao ndio watumiaji wakubwa wa teknolojia, kuhakikisha matumizi hayo yanakuwa yenye tija kwao na kwa Taifa.
“Licha ya manufaa mengi ya TEHAMA ni wazi kuwa ikitumika vibaya inaweza kusababisha madhara makubwa ikiwemo mifarakano, vurugu, machafuko, vita na kuongezeka kwa vitendo viovu kama uhalifu wa mitandao utakatishaji fedha na kadhalika,” ametahadharisha.
Amehimiza matumizi ya TEHAMA nchini na kusema kwamba katika mapinduzi ya nne ya viwanda, shughuli nyingi zikiwemo kilimo, afya, utoaji huduma zinategemema teknolojia.