Rais Samia Suluhu Hassan amesema Serikali ina mpango wa kuzalisha mbolea kuanzia tani milioni sita kwa mwaka huu hadi milioni 16 kufikia mwaka 2026.
Ameyasema hayo katika mkutano wa wakuu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliyofanyika katika ukumbi wa AICC, jijini Arusha.
Ameeleza namna soko lilivyo na umuhimu kwa chochote kinachozalishwa katika nchi, na katika mkakati wa kuisaidia Afrika Mashariki kuwa kitovu cha chakula.
Kwa upande wake Rais Uhuru Kenyatta amezitaka nchi za Afrika kungana na kujiendeleza zenyewe kwa kutumia rasilimali zilizopo ili kuzalisha utajiri kwa ajili ya watu wa Afrika na si kwa ajili ya watu wengine.
Naye mwakilishi wa Rais wa DR Congo, Waziri Mkuu, Jean-Michel Sama Lukonde amewashukuru viongozi na wanachama kuisaidia nchi yake kuingizwa kama wanachama wa saba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki na kwamba nchi hiyo iko katika majadiliano na nchi ya Kenya na Tanzania ili kuongeza uhusiano zaidi.
“Tunafanya majadiliano na Kenya na Tanzania ili tuweze kuongeza mahusiano yetu, kufungua mipaka na kuhakikisha kuna mzunguko huru wa watu na bidhaa, […] itakuza biashara na kuongeza mahusiano kati ya watu na mabadilishano ya kitamaduni” amesema.