Serikali: Mara ya mwisho mitihani kuvuja ni mwaka 2008

0
43

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga amesema suala la uvujaji wa mitihani nchini halipo, bali kinachotokea ni udanganyifu unaofanywa na wanafunzi, walimu na wasimamizi wakati wa mitihani.

Kapinga ameyasema hayo bungeni jijini Dodoma akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Husna Juma Sekiboko, aliyetaka kujua ni hatua zinazochukuliwa na Serikali kudhibiti kuvuja kwa mitihani nchini.

Kipanga amesema mara ya mwisho mtihani ilivuja mwaka 2008 ambapo ulikuwa ni mtihani wa hesabu kidato cha nne, kutoka hapo hakuna mtihani wowote uliovuja.

“Kinachotokea ni udanganyifu katika mitihani kwenye baadhi ya maeneo kwa sababu suala la mitihani ni suala la mchakato ambao unahusisha utungaji wa mitihani, ufungaji wa mitihani na usafirishaji kisha unakwenda kwenye vituo vya mitihani,” amesema.

Ameeleza matukio ya udanganyifu hutokea baada ya mitihani kufunguliwa ambapo pengine wanafunzi, walimu na wasimamizi wanaingia na nyaraka ambazo hazitakiwi kwenye chumba cha mtihani.

Spika awataka viongozi wa Serikali kuzima magari yao ili kubana matumizi ya mafuta

Ameongeza kwamba, Serikali inapambana ili kukomesha udanganyifu na wote watakaokamatwa wakifanya hivyo watachukuliwa hatua.

Hata hivyo Sekiboko ameomba Mwongozo wa Spika akisema kuwa majibu ya Naibu Waziri yana viashiria vya udanganyifu kwani mwaka 2021 yeye (Sekiboko) na wenzake walipewa kazi ya kupitia uvujaji na udanganyifu kwenye mitihani, hivyo si sahihi kusema kwamba mara ya mwisho mitihani kuvuja ni mwaka 2008.

Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson amejibu kuwa atatolea ufafanuzi baada ya kujiridhisha na kazi ambayo kamati aliyokuwemo Mbunge Sekiboko ilikwenda kufanya, lakini akasisitiza kuwa uvujaji wa mitihani ni sehemu ya udanganyifu katika mitihani.

Send this to a friend