
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mohamed Mchengerwa, amesema katika mwaka wa Fedha 2024/25, Serikali imetoa mikopo yenye thamani ya shilingi bilioni 82.84 kwa vikundi 8,275 vya wanawake, vijana, na watu wenye ulemavu kupitia mpango wa asilimia 10 ya mapato ya halmashauri.
Amesema hayo wakati akiwasilisha mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2024/25 na makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2025/26 katika vikao vya kamati za kudumu za Bunge linaloendelea jijini Dodoma.
Ameeleza kuwa kati ya fedha hizo shilingi bilioni 40.71 zimetolewa kwa vikundi 4,557 vya wanawake, shilingi bilioni 36.64 kwa vikundi 2,827 vya vijana na shilingi bilioni 5.48 kwa vikundi 891 vya watu wenye ulemavu.
Aidha, amefafanua kuwa Ofisi ya Rais – TAMISEMI imeandaa mwongozo wa ukomo wa mkopo ambao utawezesha halmashauri kusimamia utoaji wa mikopo yenye tija kwa jamii na kulingana na mwongozo huo kiwango cha juu cha mkopo kwa kikundi ni shilingi milioni 150 na kiwango cha chini cha mkopo ni shilingi 500,000.