Serikali: Minara ya simu kwenye makazi haina madhara

0
78

Wizari ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imesema kuwa minara ya simu inayowekwa katika maeneo ya wananchi haina madhara yoyote kwani ina viwango vya chini zaidi vya miale, ambavyo vipo chini zaidi ya viwango vya chini vinavyotakiwa.

Ameyasema hayo Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Kundo Mathew wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Momba, Condester Sichwale wakati akiomba Serikali kutoa mwongozo kwa kampuni za simu kuhakikisha wanapolipa pango la ardhi kwa mmiliki watoe pia asilimia kwa serikali za mitaa na vijiji ili kuondoa mgongano wa maslahi kwenye jamii.

Akijibu swali hilo Mathew amesema utoaji wa asilimia hutokana na dhana iliyojengeka kuwa minara iliyopo katika maeneo ya wananchi inawaathiri na ndiyo maana wanataka asilimia kama fidia.

“Naomba nikuhakikishie Spika na wa Bunge kuwa minara hii ina kiwango ambacho kimewekwa chini ya volti saba kwa mita ambacho ni kiwango cha chini kinachotakiwa, lakini minara yote nchi nzima iko kati ya tatu mpaka nne, hivyo ni vema kuondoa mitazamo hii,” amesema Naibu Waziri.

Hata hivyo amesisitiza makampuni ya simu kuhakikisha kuwa wanashirikisha Serikali za wilaya na vijiji wanapotaka kujenga minara ya mawasiliano katika Kijiji husika ili kuepuka migogoro baina yao, pamoja na kuingia mikataba ya ulinzi wa minara na serikali za vijiji ili kuwa na ulinzi wa uhakika.

Send this to a friend