Serikali: Mtumishi aliyekuwa anaosha vifaa vya hospitali ni jambo la kawaida

0
41

Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Jomari Satura amemvua madaraka Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya Kivule kwa kushindwa kusimamia majukumu yake hospitalini hapo.

Hatua hiyo imefuatia baada ya kusambaa kwa kipande cha video kinachoonesha mtumishi wa hospitali hiyo, Deborah Chacha akisafisha vifaa vya kuhudumia wagonjwa vya hospitali na kisha kuvianika juani.

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Mkurugenzi imesema uamuzi huo umetokana na kushindwa kuhakikisha utoaji wa huduma za afya katika kituo hicho unazingatia ubora, miongozo, taratibu na sheria za afya.

“Ofisi ya Mkurugenzi inakemea vikali vitendo kama hivi na itahakikisha havijirudii tena na kuwataka watumishi wote wa sekta ya afya na sekta nyingine kufanya kazi kwa weledi, uadilifu na kwa kuzingatia miongozo na taratibu zote,” imesema taarifa ya Ofisi ya Mkurugenzi.

Hata hivyo, Mkurugenzi amesema vifaa hivyo vilivyoonekana kupitia video hiyo havikuwa vimetumiwa na wagonjwa, na kwamba tukio lililoonekana ni jukumu la kawaida la uchambuzi na usafi wa kawaida wa vifaa hivyo kutoka stoo ya kuhifadhia vifaa.

Send this to a friend