
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali kupitia Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu ((HESLB) imetumia shilingi trilioni 8.2 kugharamia wanafunzi tangu ilipoanzishwa ambapo takriban wanafunzi 830,000 wamenufaika na mfumo huo.
Amesema hayo leo alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye kilele cha maadhimisho ya miaka 20 ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, iliyofanyika kwenye Kituo cha Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.
“Mafanikio tuliyonayo leo, ni matokeo ya utashi wa kisiasa, uongozi thabiti, maono na michango ya viongozi wetu. Viongozi wetu katika awamu zote walifanya kazi kubwa ya kuhakikisha Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu inafanya vizuri, viongozi wetu waliona mbali kuanzisha mfumo huu wa ugharimiaji wa elimu ya juu kupitia Bodi ya mikopo”
Aidha, amesema Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu imefanikiwa kukusanya fedha kiasi cha shilingi trilioni 1.5. “Ninatambua marejesho hayo yamepatikana kutokana na jitihada na ubunifu mkubwa ambao unasaidia kuwafikia wanufaika ambao wamehitimu na mikopo yao imeiva.”
Ameongeza kuwa katika kuhakikisha kuwa mikopo hiyo haiwi mzigo kwa wanafunzi, Serikali iliamua kufuta tozo za kulinda thamani ya fedha ili kuondoa changamoto katika urejeshaji wa mikopo. “Kwa sasa mnufaika anarejesha kiasi kile kile ambacho amekopeshwa kwani tozo hizo zilikuwa zinasababisha ongezeko la madeni ya mikopo hiyo.”
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda amesema wakati Rais Samia anaingia madarakani alikuta fedha zinazotolewa kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu ikiwa ni shilingi bilioni 464. “Lakini alipoingia aliagiza fedha kwa ajili ya mikopo ziongezwe, na tuliongeza hadi kufikia bilioni 570, tukaendelea hadi bilioni 654 na sasa ni shilingi bilioni 731.”