Serikali: Tunafanya juhudi kuwarejesha nyumbani Watanzania walioko Iran na Israel

0
141

Kutokana na vita vinavyoendelea kati ya Iran na Israel, Serikali ya Tanzania imesema inaendelea na juhudi za kuwaorodhesha Watanzania waliopo katika nchi hizo ili kuhakikisha raia hao wanarejeshwa nyumbani salama.

Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imesema taarifa zinaonesha kuna Watanzania 168 wako nchini Iran wakiwemo wanafunzi 134 waliopo katika Mji wa Qom na wengine 34 katika jiji la Tehran.

Kwa upande wa Israel, imesema inakadiriwa kuwa kuna Watanzania zaidi ya 200 wakiwemo watumishi wa Ubalozi wa Tanzania, wanafunzi na wafanyakazi katika taasisi mbalimbali.

Aidha, Serikali imewahakikishia wananchi kuwa Watanzania waliopo nchini Israel na Iran wako salama.

Mbali na hayo, Serikali imethibitisha kuwa jengo la Ubalozi wa Tanzania nchini Israel halijaathirika na mashambulizi ya hivi karibuni ya Iran.

“Wakati mashambulizi hayo yanatokea hapakuwa na mtu yeyote ndani ya jengo hilo na maafisa wa Ubalozi pamoja na familia zao wote wako salama,” imesema taarifa.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa balozi za Tanzania nchini Israel na Umoja wa Falme za Kiarabu zimekuwa zikiwasiliana na Watanzania waliopo katika maeneo ya Iran na Israel zikiwataka kuchukua tahadhari za kiusalama wakati Serikali ikiendelea kushughulikia masuala yanayohusu usalama wao ikiwa ni pamoja na mustakabali wao wa kurudi nyumbani.

Send this to a friend