
Serikali imesema imeanza kufanya mashauriano na Marekani ili kujua maeneo yanayohitaji kufanyiwa maboresho, hususani kwenye masuala ya kikonseli ili raia wa Tanzania wasizuiwe kuingia Marekani.
Akitoa taarifa hiyo, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema ameona tangazo la Serikali ya Marekani la kutaka kufanyiwa kazi kwa mambo kadhaa ya kiuhamiaji ambayo yanaweza kusababisha raia wa Tanzania kuzuiwa kuingia nchini Marekani.
“Naomba kuujulisha umma tayari Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje imeanza kufanya mashauriano na wenzetu upande wa Marekani kujua maeneo ambayo yanatakiwa kufanyiwa maboresho, hususani yanayohusiana na masuala ya kikonseli ili kuharakisha Tanzania isiwe moja ya nchi ambazo raia wake watazuiliwa kuingia Marekani,” amesema.
Uamuzi huo ni baada ya Serikali ya Marekani kutoa orodha ya nchi 36 ikiwemo Tanzania, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ambazo raia wake wanaweza kukutana na marufuku hiyo kwa kile ilichokieleza kuwa kukosekana kwa ushirikiano kwa baadhi ya serikali katika kutoa hati za utambulisho zenye kuaminika.