Serikali imesema kuwa walicholipwa waathirika wa mabomu ya Mbagala yaliyotokea mkoani Dar es Salaam ni kifuta machozi na sio fidia, kwa kuwa Serikali huwa haitoi fidia kwenye majanga yanayotokea.
Hayo yamesemwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene wakati akijibu swali la Mbunge wa Mbagala, Abdallah Chaurembo aliyetaka kujua kauli ya Serikali juu ya mapunjo ya fidia kwa wananchi walioathirika na mlipuko wa mabomu Mbagala.
“Huwezi ukayawekea [majanga] utaratibu wa kulipa fidia, kwa hiyo hakuna utaratibu wa fidia kwa majanga, bali ambacho hutokea Serikali huweza kutoa kifuta machozi au mkono wa pole kwa familia zilizoathirika,” amesema.
Serikali:Megawati 190 za umeme hazipatikani kutokana na upungufu wa maji
Ameeleza kuwa jumla ya TZS bilioni 17.4 zimetumika kutoa mkono wa pole kwa wananchi 12,647 walioathirika na milipuko ya mabomu yaliyotokea katika kambi ya Jeshi la Wananchi Mbagala jijini Dar es Salaam pamoja na kugharamia mazishi ya watu 29 waliofariki dunia kutokana na mlipuko huo uliotokea Aprili 29, 2009 katika kambi ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).