Serikali ya Kenya yafunga jengo la Freemason kwa kutolipa kodi

0
3

Serikali ya Kaunti ya Nairobi nchini Kenya imefunga jengo la Freemasons’ Hall la Grand Lodge of East Africa lililoko katikati ya jiji kutokana na deni la kodi ya ardhi lililofikia Ksh. milioni 19 [TZS milioni 396.6].

Operesheni hiyo imeongozwa na Mjumbe wa Kamati ya Afya katika Baraza la Mawaziri wa Kaunti, Suzanne Silantoi, ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kaunti dhidi ya wadaiwa wa kodi, aliyeongozana na maafisa wengine ambao walisema taratibu zote zilifuatwa kabla ya kufunga jengo hilo ikiwa ni pamoja na kutuma barua na kutoa ilani za madai na matangazo kwenye magazeti.

Silantoi ameongeza kuwa kaunti haitaishia kufunga majengo ya wadaiwa pekee, bali pia itazuia huduma kama maji na mifereji ya majitaka kwa wale wanaoshindwa kulipa.

Kufungwa kwa Freemasons Hall kumekuja siku moja baada ya kaunti kufunga majengo manne katika eneo la biashara jijini Nairobi kwa sababu ya kutolipa kodi ya pango. Kaunti imeahidi kuendelea na zoezi hilo kwa majengo mengine.

Freemasons Hall, ni jengo la kihistoria ambalo hutumika kwa mikutano na shughuli mbalimbali za kifreemasoni.