Serikali ya Tanzania sasa kuagiza mafuta yenyewe kutoka kwa wazalishaji

0
49

Kwa mara ya kwanza serikali ya Tanzania imeefika azma ya miaka mingi ya kununua shehena ya mafuta moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji.

Hayo yameeleezwa na Waziri wa Nishati, January Makamba ikiwa ni moja ya mafanikio ya ziara yake ya hivi karibuni katika nchi zinazozalisha mafuta kwa wingi duniani ambazo ni Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu na Algeria.

Makamba amesema Hata Oktoba 28, 2021 wakiwa ziarani waliliwezesha Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kushiriki zabuni ya kiushindani na makampuni mengine ya kimataifa ambayo kila mwezi hushiriki zabuni ya kuleta mafuta nchini. TPDC ilifanikiwa kushinda sehemu kubwa ya zabuni hiyo kwa kutoa bei ndogo zaidi ya kuagiza mafuta ya dizeli nchini kwa mwezi wa Disemba mwaka huu ambapo itapunguza makali ya bei ya mafuta ya dizeli kwa mwezi Disemba.

“Kudhihirisha kwamba hatua hii ina manufaa, kwa mfano, Agosti 2021, wakati bei ya mafuta ghafi duniani ilikuwa dola 73 kwa pipa, kampuni iliyoshinda zabuni ya kuleta mafuta ya dizeli nchini ilituuzia kwa dola 30 kwa tani za ujazo (premium). Safari hii, pamoja na bei ya mafuta ghafi duniani kupanda na kufikia dola 86 kwa pipa, TPDC italeta dizeli nchini mwezi Disemba kwa wastani wa dola 20 kwa tani za ujazo,” ameeleza Makamba.

Ametaja mafanikio mengine kwenye ziara hiyo kuwa ni:

1. Serikali kukubaliana na Serikali za nchi hizo na makampuni yao ya Taifa ya mafuta kushirikiana katika masuala ya mafuta na gesi. Katika miezi ijayo, baada ya taratibu za kiserikali na kisheria kukamilika, makubaliano hayo yenye maslahi kwa nchi yatatangazwa.

2. Serikali imefanikiwa kushawishi nchi rafiki hizo kushirikiana na Tanzania kujenga kituo kikubwa cha upokeaji na uhifadhi mkubwa wa mafuta (fuel terminal) kwa ajili ya soko la ndani ya nchi, lakini kwa mahitaji ya nchi za Afrika Mashariki na Kati na nyingine za mbali pale itakapohitajika. Kituo hicho kitatuhakikishia kuwa na kiasi cha kutosha cha mafuta ndani ya nchi wakati wote. Kwa sasa, iwapo kutatokea dharura huko duniani na Tanzania ikashindwa kuagiza mafuta, kiasi cha mafuta yaliyopo nchini yatatosheleza kwa wastani wa siku 15 tu. Mazungumzo kuhusu taratibu za kuanzisha kituo hiki yataanza mwezi wa Novemba.

3. Baada ya wiki mbili kuanzia sasa, kutakuwa na ziara za viongozi na watalaam kutoka katika nchi hizo kuja Tanzania kwa ajili ya kukamilisha taratibu za utekelezaji wa makubaliano kwenye maeneo waliyokubaliana kushirikiana. Wizara ya Nishati itaendelea kuratibu na kufuatilia ili kuhakikisha kwamba mafanikio yaliyopatikana kwenye ziara hiyo yanadumu na makubaliano na nchi hizi rafiki yanatekelezwa kwa maslahi mapana ya Tanzania na watu wake.

 

Send this to a friend