Serikali ya Zanzibar yalaani unyanyasaji unaofanyika kwa sababu za kidini

0
31

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imelaani vitendo vya unyanyasaji vinavyoendelea kufanyika sehemu mbalimbali visiwani humo katika kipindi hiki cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan, ikisema kadhia hiyo ni kinyume na misingi ya kuvumiliana katika imani za kidini.

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema ina mamlaka ya kuilinda Katiba ya nchi na watu wake, hivyo hatua yoyote ile yenye kuhatarisha umoja, amani na mshikamano haitavumiliwa.

“Zanzibar ni nchi yenye historia kongwe ya uvumilivu wa kidini ambapo Uislamu na Ukristo uliingia mapema kuwa sehemu muhimu ya utamaduni uliodumu kwa karne nyingi. Hii inatufundisha kuhusu ustaarabu wa Wazanzibar kuvumiliana kidini na ndio msingi wa mshikamano miongoni mwetu,” imeeleza taarifa.

Aidha, imeongeza kuwa Serikali itaendelea kulinda haki na uhuru wa mtu kuabudu kama ilivyoelezwa katika Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984, na kuwahimiza wananchi kujizuia kwa namna yoyote ile kuingilia uhuru wa mtu binafsi kuabudu.

Hata hivyo, imewataka wananchi kuendelea kudumisha amani na upendo kama ambavyo mafundisho ya dini yanavyosema, na kwamba tofauti za kidini zisiwe chanzo cha kuvuruga amani, umoja na mshikamano.

Send this to a friend