Serikali yaagiza mafuta ya mikoa ya Kaskazini kuchukuliwa Bandari ya Tanga
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imewaagiza wasambazaji wa bidhaa za petroli katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara kuchukua bidhaa hizo kutoka Bandari ya Tanga, na si sehemu nyingine.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa EWURA inaeleza kuwa utaratibu wa wafanyabiashara hao kuchukua mafuta kutoka Bandari ya Dar es Salaam kunawaathiri wafanyabiashara wa jumla walioingiza mafuta kupitia Bandari ya Tanga.
Aidha, amesema utaratibu huo unadhoofisha jitihada za serikali za kupunguza gharama za ufanyaji biashara nchini ambapo mteja wa mwisho angenufaika zaidi.
EWURA imesema msambazaji yeyote ambaye atakiuka agizo hilo atatozwa faini isiyopungua TZS milioni 100 au kifungo jela kisichopungua miaka 10 au vyote.
Mamlaka hiyo imeeleza kuwa itafuatilia kwa karibu usambazaji wa nishati hiyo nchini ili kuhakikisha maslahi ya wadau wote (wateja, wafanyabiashara wa jumla na rejareja na serikali) yanalindwa.