Serikali yaanza biashara ya kuuza mafuta (dizeli, petroli)
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amezindua rasmi biashara ya kuuza na kusambaza mafuta nchini kwa kufungua kituo cha kwanza kuuza mafuta ya Petroli na Dizeli cha Serikali kitakachosimamiwa na Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC) kupitia Kampuni yake Tanzu ya Mafuta ( TANCOIL).
Aidha Dkt. Kalemani amesema kuwa kuzinduliwa na kufunguliwa kwa biashara hiyo ni kutimiza azma na nia njema ya Serikali ya kuboresha shirika la TPDC, kuwapatia na kuwasogezea karibu wananchi wake huduma ya kupata mafuta yenye viwango vya ubora unaotakiwa, bei nafuu, na yatakayopatikana kwa wingi muda wote.
Amesema TPDC kupitia TANCOIL itashirikiana na halmashauri zote nchini kuhakikisha inafanikisha azma ya Serikali ya kufungua na kuweka vituo vya kuuza na kusambaza mafuta katika kila halmashauri nchini pamoja na miundombinu ya kuhifadhi na kusafirisha mafuta.
“Tumeshaanza biashara ya kuwauzia wananchi wetu mafuta, sitegemei kusikia mafuta yanauzwa kwa bei ghali katika vituo vya serikali. TPDC na TANCOIL mnielewe vizuri hapa! hii haipo na haitakuwepo,” amesema kiongozi huyo.
Ameongeza kuwa serikali kupitia TPDC itajenga vituo 100 kwa kipindi cha miaka 5 ijayo, tayari baadhi ya Halmashauri zimeanza kutenga maeneo yatakayojengwa vituo hivyo, na itahakikisha kuwa nusu ya mafuta yote yanayoingizwa nchini yanasimamiwa TPDC.