Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji amesema Serikali imefufua majadiliano na wawekezaji watakaondeleza mradi wa Bandari na Kanda Maalum ya Kiuchumi Bagamoyo (BSEZ) utakaowezesha nchi kukabiliana na kasi ya ushindani wa biashara, na shughuli za uchumi.
Akizungumza hapo jana Bungeni jijini Dodoma alipokuwa akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake mwaka wa fedha 2022/2023, amesema wizara imefufua majadiliano na wawekazaji wa Kampuni za China Merchants Holdings (International) CO. Ltd (CMHI) na Oman Investment Authority (OIA).
“Majadiliano hayo yanahusu eneo dogo la Mradi wa BSEZ kwa kuendeleza eneo la hekta 3,087 kati ya hekta 9,887 unahusisha ujenzi wa bandari na kituo cha usafirishaji (Logistics Park) kwenye eneo la hekta 887 na uendelezaji wa eneo maalum la viwanda (Portside Industrial City) kwenye eneo la hekta 2,200,” amesema.
Aidha, ameeleza kwamba uwekezaji katika maeneo ya mradi utafanywa kwa kuvutia wabia wa sekta ya umma na sekta binafsi au kufanywa na mwekezaji binafsi.