Serikali yabainisha vyanzo vitakavyogharamia bima ya afya kwa wasio na uwezo

0
37

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema kwa mara ya kwanza Rais Samia Suluhu Hassan anaweka historia na msingi wa kuhakikisha Watanzaia wasio na uwezo takribani milioni 15.8, sawa na kaya milioni 3.6, wanakwenda kupatiwa bima ya afya bila malipo ili kuweza kumudu gharama za matibabu.

Ameyasema hayo leo bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha Muswada wa Bima ya Afya kwa Wote ambao ulikwama mwezi Februari mwaka huu kwa hoja iliyotolewa na Bunge ya kutokuwepo kwa chanzo endelevu cha fedha za kutekeleza mpango huo.

Waziri Ummy amesema kutokana na upekee wa Bima ya Afya kwa Wote, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha wamependekeza baadhi ya vyanzo vya mapato vya kuendesha mfuko huo ili kugharamia bima ya afya kwa watu wasio na uwezo.

Maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi Tanzania yanapungua

“Vyanzo hivyo ni pamoja na sehemu ya mapato yatokanayo na ushuru wa bidhaa kwenye vinywaji vyenye kaboni, vinywaji vikali, bidhaa za vipodozi, kodi ya michezo ya kubahatisha, ada ya bima za vyombo vya moto na mapato yatokanayo na ushuru wa miamala ya kielektroniki kwa kadiri itakavyopendekezwa na waziri mwenye dhamana na masuala ya fedha, fedha zitakazotengwa na bunge, mapato yatokanayo na uwekezaji wa mfuko na zawadi pamoja na misaada kutoka kwa wadau mbalimbali,” amebainisha

Aidha amesema ni asilimia 15 pekee ya Watanzania ambao wana bima huku wengi wanaojiunga na bima kwa hiari wakiwa ni wangonjwa, hivyo ameeleza kuwa Serikali itaendelea kuwahimiza na kutoa elimu kwa wananchi ili watambue umuhimu wa bima ya afya.

Send this to a friend