Serikali Yachukua Hatua Kali Kudhibiti Migogoro ya Ardhi Dar es Salaam

Migogoro ya ardhi katika Dar es Salaam imeendelea kuibua changamoto kwa wananchi, hali iliyolazimisha Serikali kuchukua hatua za kuimarisha usimamizi na utatuzi wa migogoro hiyo ili kulinda amani na utulivu wa jamii.
Akizungumza wakati wa ziara ya kusikiliza kero za wananchi katika Mtaa wa Nyakasangwe, Kata ya Wazo, Wilaya ya Kinondoni, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila amesema migogoro mingi inasababishwa na kutokuheshimu taratibu za kisheria pamoja na maamuzi ya vyombo vya dola.
Amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kuheshimu maamuzi yanayotolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania katika mashauri ya ardhi, akibainisha kuwa kufanya hivyo kutapunguza migogoro isiyo ya lazima na kuimarisha amani katika jamii.
Aidha, aliwaonya baadhi ya viongozi wa Serikali za Mitaa wanaodaiwa kushiriki kughushi nyaraka zinazochochea migogoro hiyo, akisema mihuri waliyopewa inapaswa kutumika kwa uadilifu na kwa maslahi ya umma, vinginevyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Katika hatua ya kurejesha haki, Chalamila alimkabidhi Glory Mnisi shilingi milioni 5 baada ya kudhulumiwa eneo alilonunua, fedha zilizorejeshwa kufuatia uingiliaji wa ofisi ya Mkoa, huku mwananchi huyo akiishukuru Serikali kwa kumsaidia kupata haki yake.
Pia, ameagiza kuundwa kwa kamati maalumu ya kuchunguza migogoro ya ardhi katika maeneo husika na kusisitiza umuhimu wa mabaraza ya ardhi kupewa mafunzo ya mara kwa mara ili kuimarisha utatuzi wa migogoro na kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi.








