Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amelielekeza Baraza la Madaktari Tanganyika (MCT) na Baraza la Wauguzi na Wakunga Tanzania (TNMC) kuhakikisha ndani ya siku saba liwe limetoa taarifa ya tukio la kifo cha mjamzito na mtoto wake kilichotokea Novemba 11, 2023 mkoani Tanga.
Amesema tayari hatua za awali zimeshachukuliwa ikiwemo kutuma timu kutoka Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa inayojumuisha madaktari bingwa wawili akiwemo Daktari Bingwa wa Wanawake na Uzazi na Daktari Bingwa wa Huduma za Usingizi ili kufanya uchunguzi wa tukio hili.
“Hatua nyingine iliyochukuliwa baada ya tukio hilo ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni kuwasimamisha kazi watumishi watatu walioshiriki kumpatia huduma mama huyo tangu alipopokelewa kituoni hadi umauti ulipomkuta ili kupisha uchunguzi wa tukio hili baya na lisilopaswa kuvumiliwa,” amesema.
Aidha, amewahakikishia Watanzania kuwa baada ya kupokea taarifa ya uchunguzi, kila mtumishi aliyehusika atachukuliwa hatua kali za kitaaluma, kiutumishi na kijinai ikiwemo kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma za kijinai pale itakapothibitika.