Serikali imesema ajali ya meli ya mizigo iliyosajiliwa na Tanzania ambayo imezama katika bandari ya Assaluyer Kusini mwa Iran Jumatatu jioni ilisababishwa na upakiaji usiofaa wa makontena.
Kwa mujibu wa gazeti la The Citizen, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Majini Zanzibar (ZMA), Sheikha Mohamed amesema mara baada ya kupata taarifa hizo, mamlaka hiyo iliamuru mpelelezi wa ajali za baharini ambao makao yao makuu ni Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kwenda eneo la tukio na kuandaa ripoti ya ajali hiyo.
Bi. Mohamed ameongeza kuwa meli hiyo inayotambulika kwa jina la ‘Anil’ inayosafiri chini ya bendera ya Tanzania, inamilikiwa na Amir Kashiani wa Iran chini ya shirika linalotambulika kwa jina la ‘Royal Classification Society’.
Angalia matokeo ya Kidato cha Nne mwaka 2022
Shirika rasmi la habari la IRN limeripoti kuwa meli hiyo ilipinduka kwa sababu kontena zilizokuwa ndani yake ziliwekwa vibaya kwenye gati nambari 9 ya bandari.
Picha zilizosambaa baada ya tukio hilo zinaonesha chombo hicho kikizama ubavuni huku makontena yakielea pembeni yake.