Serikali yaeleza sababu ya bei ya saruji kupanda

0
46

Serikali imesema saruji kupanda bei kumechangiwa na mambo kadhaa ikiwa ni pamoja ni baadhi ya viwanda kufungwa kwa ajili ya matengenezo.

Akizungumza na TBC, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Ludovick Nduhiye amesema kufungwa kwa viwanda hivyo kumeathiri viwanda vingine kwani hutegemeana katika kupata malighafi za kuzalisha saruji.

Amesema miaka ya nyuma ilizoeleka kwamba kipindi cha uchaguzi miradi ya serikali inasimama ndio sababu viwanda vilitumia muda huo kwa matengenezo, lakini mwaka huu imekuwa tofauti, miradi yote mikubwa, ujenzi wa reli, barabara, bwawa la Nyerere imeendelea.

“Bwawa la kuzalisha umeme la Mwalimu Nyerere linahitaji takribani tani elfu 10 hadi elfu 20 kwa mwezi.”

Aidha, amesema sababu nyingine ni kuongezeka kwa matumizi ya bidhaa hiyo muhimu katika ujenzi. Amesema kwa mwaka 2014/15, mahitaji ya ndani yalikuwa chini ya tani milioni 4 kwa mwaka lakini hadi sasa mahitaji ya ndani yamefikia tani milioni 6 kwa mwaka.

Amesema pia baadhi ya viwanda vinazalisha chini ya uwezo wake akitolea mfano kiwanda cha Dangote ambacho kina uwezo wa kuzalisha tani milioni 3 kwa mwaka lakini sasa wanazisha tani milioni 1.2 kwa mwaka, na hivyo kupelekea upungufu.

Kuhusu kudhibiti bei amesema kuwa Tume ya Ushindani imeanza kufuatilia kuona kama kuna watu wanahujumu kwa kuficha bidhaa hiyo ili kutengeneza upungufu kwa manufaa yao.

Send this to a friend