Serikali yafunga vituo 74 vya kutibu waathirika wa corona

0
43

Serikali imeendelea kufunga kambi/vituo vilivyokuwa vinatumika kwa ajili ya kuwaweka na kuwatibu watu wenye maambukizi ya virusi vya corona nchini, ambapo hadi sasa kambi 74 tayari zimefungwa.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu ameeleza hayo wakati alipotembelea kukagua Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Lulanzi, ambayo ilikuwa ikitumiwa kutibu waathirika wa COVID19.

Akiwa kambini hapo Waziri Ummy ameagiza hospitali hiyo kurejea kutoa huduma kama kawaida kwa wananchi kwa sababu ni salama na hakuna mgonjwa yeyote wa corona, na kwamba mgonjwa wa mwisho aliruhusiwa Mei 26 mwaka huu.

“Hivi sasa Hospitali ya Lulanzi, si hospitali au kambi kwa ajili ya wagonjwa wa corona. Mgonjwa wa mwisho alitoka hapa tarehe 26 Mei,” amesema Ummy.

Amewataka wananchi kutokuwa na hofu, badala yake waende hospitalini hapo kupata matibabu kwani huduma zinatolewa.

“Tulikuwa na hospitali au kambi 85, leo hii [jana] zimebaki kambi 11 tu,” ameeleza kiongozi huyo.

Serikali ya Tanzania imeondoa mazuio mbalimbali iliyokuwa imeyaweka kama njia ya kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona yakiwemo kuruhusu shughuli za michezo, kufungua taasisi za elimu pamoja na kufungua anga kwa ajili ya safari za ndege.

Send this to a friend