Serikali yafuta tozo 42 kati ya 47 zao la Kahawa

0
54

Serikali imefuta tozo 42 kati ya 47 ambazo walikuwa wanatozwa wakulima wa kahawa wa Mkoa wa Kagera, hivyo kubakisha tozo 5 tu ambazo zitakuwa ni jumla ya TZS 267 kwa kila kilo ya kahawa, kutoka TZS 830 za awali.

Uamuzi huo umetolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na kuwaagiza viongozi wa vyama vya Ushirika, wasimamie vyama vyao kwa uaminifu na weledi ili vilete tija kwa wakulima, na kuacha tabia ya kukopa pesa benki kwa ajili ya kununua kahawa kwa wakulima.

Aidha, amesema kuanzia sasa mauzo ya kahawa katika mkoani humo yatafanyika kwa njia ya mnada utakaofanyika kwenye ngazi ya vyama vya msingi.

Kwa upande wake Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amevionya baadhi ya vyama vya ushirika kuacha kuwaumiza wakulima wa kahawa kwa kuwaongezea tozo zisizokuwa na tija na kucheleweshewa malipo.

Waziri huyo amemuagiza Mkurugenzi wa Bodi ya Kahawa kugawa miche ya kutosha ya kahawa kwa wakulima ili ilete tija na kuwaongezea kipato.

Amesema ili kuhakikisha maafisa ugani wanatekeleza majukumu yao ipasavyo Wizara imeandaa utaratibu wa kutoa usafiri pamoja na vifaa vya kupimia udongo.

Katika msimu wa kilimo wa mwaka 2021/2022 mkoa huo ulizalisha tani 52,000 za kahawa ya maganda zilizokuwa na thamani ya TZS bilioni 69.

“Bei ya kahawa imeendelea kuimarika kwani katika msimu huu wakulimwa walilipwa TZS 1,300 kwa kilo moja ya kahawa ya maganda na TZS 3,300 kwa kilo moja ya kahawa hai (Organic cofee),” amesema Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Prof. Faustin Kamuzora.

Send this to a friend