Serikali yaja na mbinu za kuongeza akiba ya dola nchini

0
53

Kutokana na upungufu wa dola unaozikumba nchi mbalimbali hivi sasa, Serikali imesema imeanza kutekeleza sera ya fedha ya kununua dhahabu kupitia Benki Kuu ya Tanzania ili kupata dola kwa ajili ya kuongeza dola nchini.

Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema kukosekana kwa dola nchini kumetokana na sababu mbalimbali ikiwemo janga la UVIKO-19 ambalo lilizuia watu kufanya uzalishaji katika maeneo mbalimbali duniani, vita vya Ukraine na Urusi pamoja na mabadiliko ya tabia ya nchi.

Ameeleza kuwa sababu nyingine ni Marekani kupandisha riba ya hati fungani hadi kufikia zaidi ya asilimia 5, hali iliyopelekea watu waliokuwa na dola maeneo mbalimbali kwenda kununua hati fungani, hatua mabayo imerejesha dola nchini humo.

“Nchi iliyowekewa vikwazo vikubwa ni Urusi, moja kati ya maeneo ambayo Urusi imeathirika ni bidhaa ambazo Urusi ilikuwa ikizalisha kwenda nchi mbalimbali zikawa haziendi, kwahiyo nchi mbalimbali zimeingia kwenye presha kubwa ya kutafuta bidhaa hizo, ama kuongeza uzalishaji kwenye maeneo mengine. Tanzania imejikuta ikitumia dola za kimarekani kwa kiasi kikubwa kwenye soko,” ameeleza.

Fahamu kuhusu ukosefu wa Dola unavyoweza kuathiri uchumi

Ameongeza kuwa moja ya vitu ambavyo Tanzania inahitaji ili kuongeza fedha za kigeni hususani dola ni kuongeza mauzo ya nje, hivyo Serikali imechukua hatua ya kuhakikisha inawasaidia wawekezaji waweze kuongeza uzalishaji ndani ya nchi ili kuongezeka kwa fedha hizo.

Aidha, Msigwa amesema Serikali imeanza kutoa leseni kwa maduka ya kubadilisha fedha yaliyokuwa yamefungiwa kutokana na ukiukwaji wa taratibu, na kwamba tayari shilingi bilioni 9 za wafanyabiashara hao ambazo zilikamatwa katika oparesheni hiyo zimekwisharudishwa.

“Hapo katikati maduka ya kubadilishia fedha yalikuwa yamefungiwa kwa sababu kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu, lakini baada ya Serikali kuweka taratibu vizuri na kuimarisha masharti ya leseni, sasa hivi tumeshaanza kutoa leseni, takribani leseni 80 za maduka ya kubadilisha fedha zimekwishatolewa,” amesema Msigwa.

Send this to a friend