Serikali yakanusha ajira kupungua serikalini na sekta binafsi

0
41

Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) inakanusha habari iliyosambazwa katika baadhi ya mitandao ya kijamii hususan Jamii Forum yenye kichwa cha habari “NBS yakiri ajira sekta binafsi zimepungua kwa 42.6%, Serikalini zimepungua kwa 78.1% ndani ya mwaka mmoja.”

Habari hii imepotosha kuhusu kupungua kwa ajira Serikalini na hivyo jamii inaombwa kuipuuza kwa kuwa haina ukweli wowote.

Ifahamike kwamba, wakati NBS ikijiandaa kufanya utafiti wa Watu wenye Uwezo wa Kufanya Kazi (Intergrated Labour Force Survey) utakaofanyika mwaka 2019/20, ilifanya maoteo mwaka 2018 (projections) ya mwenendo wa hali ya Soko la Ajira Nchini ambayo yanabainisha mabadiliko yaliyotokea katika soko la ajira tangu mwaka 2014 hadi mwaka 2018. Taarifa hii inapatikana kwenye tovuti ya NBS (www.nbs.go.tz – Tanzania in Figures 2018 Uk. 40).

Maoteo ya takwimu hizo yanaonesha kuwa, idadi ya watu walio na ajira imeongezeka kutoka milioni 20.0 mwaka 2014 hadi milioni 22.0 mwaka 2018.

Aidha, takwimu zilizowekwa kwenye Tanzania in Figure 2018 Uk. 41 zinazotokana na taarifa za kiutawala (administrative records) ambazo zinasaidia kupata takwimu za ajira ambazo hazikusanywi kwenye tafiti za kawaida. Takwimu hizi hutumika pia kama kigezo cha kufanya maoteo ya hali ya ajira (proxy indicators) katika vipindi ambavyo hakuna tafiti zilizofanyika ili kutoa hali ya soko la ajira katika vipindi vifupi vifupi.

Tafsiri halisi ya Jedwali lililopo uk. 41 wa Tanzania in Figures ni kwamba, mwaka 2017/18 kulikuwa na jumla ya ajira 552,063 zilizozalishwa nchini ikilinganishwa na ajira 453,466 kwa mwaka 2016/17. Hili ni ongezeko la ajira 98,597 sawa na asilimia 21.7 kati ya mwaka 2016/17 na mwaka 2017/18.

Kati ya ajira 552,063 zilizozalishwa nchini mwaka 2017/18, ajira 415,009 sawa na asilimia 75.0 zilikuwa ni ajira kutoka Serikalini; ajira hizi zinajumuisha ajira 18,000 kutoka Serikali Kuu na ajira 397,009 kutoka katika miradi ya maendeleo kupitia Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa mwaka 2016/17 hadi 2020/21.

Hali hii inatokana na ukweli kuwa, wananchi wengi huajiriwa kwenye miradi ya kimkakati ya maendeleo inayoendelea hapa nchini ambapo Serikali imejikita kwa dhati kuitekeleza kwa ajili ya kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 na kupunguza umaskini. Kwa upande

1

mwingine, ajira 137,054 sawa na asilimia 25.0 ya ajira zote zilizozalishwa na Sekta Binafsi zimepungua kutoka ajira 239,017 mwaka 2016/17 hadi ajira 137,054.

Hivyo, hali halisi kwa jedwali hilo ni kuongezeka kwa ajira Serikalini kutoka 214,449 mwaka 2016/17 hadi 415,009 mwaka 2017/18 sawa na ongezeko la ajira 200,560 (asilimia 94) ya ajira zilizozalishwa mwaka 2016/17.

Ikumbukwe kwamba, Ofisi ya Taifa ya Takwimu hutumia taarifa za kiutawala za ajira kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu; Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu kubaini kiwango cha ajira zilizozalishwa kwa kila mwaka. Huu ndio uzoefu wa nchi nyingi duniani hususan nchi za Afrika.

Utafiti wa Watu wenye Uwezo wa Kufanya Kazi hufanyika kila baada ya miaka mitano ambapo kwa mara ya mwisho ulifanyika mwaka 2014 wakati Utafiti wa Ajira na Mapato katika Sekta Rasmi hufanyika kila mwaka na kwa mara ya mwisho ulifanyika mwaka 2016.

Takwimu hizi za ajira hukusanywa na viashiria mbalimbali vya ajira (Labour Market Indicators) na hutolewa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na Shirika la Kazi Duniani (ILO) zikiwa na lengo la kufuatilia na kutathmini sera zilizowekwa na Serikali katika Soko la Ajira.

Mwisho, Ofisi ya Taifa ya Takwimu inausisitiza Umma kupuuza habari hiyo potofu ya kupungua kwa ajira Serikalini na inatoa wito kwa wananchi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na maarifa zaidi ili kuunga mkono juhudi zinazoendelea za kujenga uchumi. Aidha, NBS inawaasa wachambuzi wote kufuata matakwa ya Sheria ya Takwimu ya mwaka 2015 kila wanapofanya uchambuzi wa takwimu mbalimbali.

Imetolewa na: Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS),

DODOMA.

14 AGOSTI, 2019

Send this to a friend