Kamishna Msaidizi wa Idara ya Uchambuzi wa Sera wa Wizara ya Fedha na Mipango, William Mhoja amesema Serikali haina malengo ya kutoza wananchi kodi au tozo kwa ajili ya kuwapa mzigo, bali inalenga kuwahusisha Watanzania wote kwa umoja katika juhudi za kujikwamua kimaendeleo.
Ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hatua ya Serikali ya kufuta baadhi ya tozo za miamala ya kieletroniki, ikiwemo huduma za kuhamisha fedha kutoka benki kwenda mitandao ya simu na tozo ya kuhamisha fedha kutoka benki moja kwenda nyingine kuwa yamefanyiwa kazi.
“Serikali imechuka hatua baada ya kupokea ushauri na maoni ya wadau wakiwemo mabenki, wananchi na wadau wengine, na hii imepelekea kufutwa kwa tozo na kupunguza gharama ya miamala kwa asilimia 10 hadi 50 kuligana na kundi la muamala husika,” amesema Mhoja.
Ameongeza kuwa utekelezaji wa uamuzi huo utaanza Oktoba Mosi mwaka huu na kuwataka wananchi kuendelea kulipa kodi ili Serikali ikusanye mapato yake na kuyatumia kutekeleza miradi ya maendeleo kwa wananchi na kwamba wanaendelea kupokea ushauri kuhusu tozo mbalimbali zinazotozwa na serikali na kwamba marekebisho mbalimbali yanaendelea kufanyika.
Amefafanua kuwa Serikali imesamehe tozo ya miamala ya kwenye utoaji wa fedha taslimu kupitia wakala wa benki, na mashine za kutolea fedha (ATM) kwa miamala yenye thamani isiyozidi Sh 30,000.