Serikali yakataza wafugaji kuweka alama kwenye ngozi za mifugo, hasa ng'ombe
Serikali amewakataza wafugaji kuweka alama kwenye ngozi za mifugo yao hasa ng’ombe kwani kufanya hivyo kunashusha thamani ya ngozi za Tanzania, na badala yake imewataka waweke alama za hereni kwenye masikio ya mifugo yao ili kulinda ubora wa ngozi za mifugo yao.
Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alipokuwa akizungumza mara baada ya kukagua ujenzi wa Mchinjio ya Vingunguti ambaopo alibainisha kuwa alama hizo kwenye ngozi za mifugo zinafanya thamani ya ngozi kutoka nchini kuwa chini.
Amesema Serikali tayari imekwishampata mwekezaji kutoka Misri ambaye amekubali kuwekeza kwenye kiwanda cha ngozi cha Mwanza hatua ambayo italihakikishia Taifa soko la ngozi.
Kuhusu ujenzi wa machinjio hiyo Waziri Mkuu amemtaka mkandarasi ahakikishe kwamba anakamilisha ujenzi huo mwishoni mwa mwezi huu kama alivyoamriwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli.
Amesema amefurahishwa na hatua ya mkandarasi huyo ambaye ni Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) ya kuongeza idadi ya watalaam na mafundi ili kuhakikisha kwamba kazi hiyo inafanyika haraka na kukamilika kwa wakati ulioamriwa na Rais Magufuli yaani Desemba 30, mwaka huu.
Waziri Mkuu Majaliwa amemtaka Mshauri Mwelekezi wa mradi huo ambaye ni M/SCONS AFRIKA LIMITED na FB Consultant wa Dar es Salaam asimamamie kwa karibu ili kujiridhisha kuwa maelekezo yote yaliyopo kwenye michoro ya ujenzi huo yanazingatiwa na mkandarasi.
Amesema Serikali imeamua kujenga machinjio hayo ya kisasa ya Vingunguti baada ya kugundua kwamba wafanyabiashara wa mifugo na mazao yake katika machinjio hayo, walikuwa wakifanya kazi zao kwenye mazingira duni na kwamba nyama iliyokuwa ikitoka kwenye machinjio hayo ilikuwa haikubaliki kwenye soko la nje ya nchi.
“Uamuazi wa Serikali kujenga machinjio haya, utaifanya nyama inayotoka hapa ikubalike kwenye masoko ya nje ya nchi, hatua ambayo itaongeza mzunguko wa fedha kwenye eneo hili wakati Serikali na Manispaa watanufaika kwani kutakuwa na ongezeko la makusanyo ya kodi,” aliongeza Mheshimiwa Majaliwa.