Serikali yamjibu Harmonize kuhusu kuanzishwa tuzo za sanaa

0
45

Serikali imesema kuwa inaendelea na mchakato wa kuanzisha tuzo kwa ajili ya wasanii wa Tanzania ambazo hazitahusu wanamuziki pekee, bali pia tasnia nyingine za sanaa ikiwemo habari na utamaduni.

Akizungumza na TBC1, Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa, Godfrey Mngereza amesema kuwa Julai 1 mwaka huu taasisi hiyo ilikutana na wasanii mbalimbali ambapo walijadili kuhusu namna ya kurejesha tuzo za sanaa zilizokuwa zikitolewa na serikali.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Sanaa, Dkt. Emanuel Ishengoma amesema Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo inaendelea na maandalizi ya tuzo hizo na kwamba wazo lililotolewa na Harmonize limewakuta tayari wameshaanza utekelezaji.

“Ndugu yangu Harmonize asiwe na wasiwasi, hatua za mwanzo tayari zimekwisha fanyika na tunasubiri tu kwenda kwao nao watoe mapendekezo,” amesema Ishengoma akizungumza na TBC.

Kauli za viongozi hao zimekuja siku chache baada ya mwanamuziki Harmonize kuandika ujumbe kupitia ukurasa wake wa Instagram akikosoa mfumo mzima wa namna tasnia ya muziki inavyokwenda nchini.

Katika ujumbe wake huo, Harmonize alieleza kuwa kwa sasa hivi ubora wa muziki umesahaulika badala yake kipimo kinachotumika kutambua msanii gani ni bora kuliko mwingine ni idadi ya video zake kutazamwa mitandaoni, hali ambayo inahatarisha ukuaji wa tasnia hiyo kwani wasanii hawatungi nyimbo bora bali wanakazana na wafuasi wa mitandaoni.

Send this to a friend