
Naibu Rais wa Kenya, Kithure Kindiki na Waziri wa Usalama wa Ndani, Kipchumba Murkomen, wamemtaka Kiongozi wa Chama cha Democracy for Citizens (DCP), Rigathi Gachagua, kutoa maelezo kwa polisi mara atakaporejea nchini, kufuatia kauli zake nchini Marekani kuhusu ugaidi.
Akiwa kwenye ziara yake nchini Marekani, Gachagua amedai kwamba Rais William Ruto lazima awaeleze Wakenya kwa nini alikutana usiku na viongozi watatu wa kundi la kigaidi la Al-Shabaab mjini Mandera kujadili masuala ya kibiashara.
Pia, amekosoa hatua ya serikali kuondoa sharti la uhakiki wa wasio Wakenya kabla ya kupewa vitambulisho, akisema inaweza kurahisisha usajili wa magaidi na kuwatambulisha kama raia wa Kenya, jambo linaloweza kuhatarisha usalama wa Marekani na dunia nzima.
Murkomen, amemshutumu Gachagua kwa kuzungumzia masuala nyeti ya usalama wa taifa kwa namna ya kisiasa, akisisitiza kuwa yanahitaji heshima na umakini wa hali ya juu. Amemtaka Gachagua awasilishe taarifa alizodai anazo ili kusaidia kuzuia mashambulizi.
“Naibu Rais wa zamani, ulipokuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, ulijiheshimu na kuilinda nchi. Lakini sasa unazungumzia ugaidi kana kwamba ni mchezo, tena ukiwa nchi ya kigeni kwa maslahi ya kisiasa,” amesema Murkomen.
Kwa upande wake, Naibu Rais Kindiki ameonya viongozi wasitumie nafasi zao kuhujumu usalama wa taifa, akisisitiza kuwa Kenya imepata majeraha makubwa kutokana na mashambulizi ya kigaidi na wizi wa mifugo kwa miaka mingi.
Gachagua ameanza ziara yake Marekani Julai 11, 2025, na tayari ametembelea majimbo kadhaa kukutana na wadau wa kimataifa, kufungua ofisi za chama chake kwa wanadiaspora, na kutafuta uungwaji mkono kwa upinzani.








