Serikali yamwajiri Mariam anayekumbatia watoto njiti

0
98

Serikali imetoa ajira ya mkataba kwa Mariam Mwakabungu anayejitolea kukumbatia watoto njiti waliotelekezwa katika Hosptali ya Rufaa ya mkoa Amana jijini Dar es Salaam, ikiwa ni siku moja tangu Rais Samia Suluhu Hassan kumzawadia shilingi milioni 2.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema Serikali itamshauri binti huyo mwenye umri wa miaka 25 ajiendeleze kielimu ili aweze kupata sifa ya kuajirika kwa kuwa hana taaluma ya uuguzi.

“Tutampa ajira ya mkataba kwanza, changamoto iliyopo bado hana sifa za kuajirika, tutamshauri ajiendeleze kielimu ili aweze kupata sifa za kuajirika Serikalini.

“Madaktari wanasema yule mama anajitoa na anapenda kufanya hiyo kazi, ana moyo yaani ni kitu anapenda, sasa kwa sababu hajasomea uuguzi itabidi aingizwe katika utaratibu huo ili aweze kupata sifa,” amesema Waziri Ummy.

Rais Samia amzawadia milioni 2 mwanamke anayejitolea kuwakumbatia watoto njiti

Aida, amesema kutokana na kwamba umri wake bado unaruhusu kuingia darasani, Waziri Ummy ameshauri kuwa ni vyema binti huyo akisomea uuguzi ngazi ya astashahada ili akawe muuguzi wa watoto njiti.