Serikali yapandisha kima cha chini cha mshahara Sekta Binafasi

0
122

Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) imetangaza kima kipya cha chini cha mshahara kwa sekta binafsi, ambacho sasa kitaanza kuwa Shilingi 358,322 kutoka Shilingi 275,060, ikiwa ni ongezeko la asilimia 33.4.

Kima hicho kipya kitaanza kutumika rasmi Januari 1, 2026. Hatua hii inakuja miezi michache baada ya Serikali kupandisha kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma kwa asilimia 35.1, kutoka Shilingi 370,000 hadi Shilingi 500,000, tangazo lililotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) mwaka huu.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete, amesema hatua hiyo ni utekelezaji wa takwa la kisheria, ambapo kima cha chini cha mshahara hupitiwa kila baada ya miaka mitatu.

Aidha, Kikwete ametoa rai kwa waajiri wote wa sekta binafsi kuzingatia na kutekeleza kima hiki kipya cha mshahara kwa kuwa ni amri ya kisheria.

Ameongeza kuwa ofisi yake haitasita kuchukua hatua kwa waajiri watakaoshindwa kutekeleza maagizo hayo, na itaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wake, kutoa elimu kwa waajiri na wafanyakazi, pamoja na kufanya tathmini za mara kwa mara kuhakikisha maagizo hayo yanatekelezwa kikamilifu.

Send this to a friend