Serikali yapinga kuilipa kampuni ya Indiana Resources bilioni 260

0
56

Serikali imewasilisha pendekezo katika Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID) la kufuta hukumu iliyotolewa Julai 14 mwaka huu inayoelekeza kulipa fidia ya Dola milioni 109 (TZS billioni 260) kwa kampuni ya Indiana Resources.

Pingamizi hilo lililobeba hoja zaidi ya 15 linaomba pia zuio la kuanza utekelezaji wa hukumu hiyo inayoielekeza Serikali kuanza kulipa kuanzia Julai 14, ikiendana na ongezeko la asilimia mbili kila siku hadi itakapomaliza malipo yote.

Indiana inanufaika na fidia hiyo kutokana na umiliki wa asilimia 62.4 ya hisa za kampuni mbili (Ntaka Nickel Holdings Ltd na Nachingwea UK Limited) zilizokuwa zikimiliki leseni ya kuhodhi ardhi katika eneo la mradi wa Nikel wa Ntaka Hill, uliokuwa Wilaya ya Nachingwea

Kwa mujibu wa hukumu hiyo, Serikali italipa baada ya mwekezaji kudai kupata hasara itokanayo na uamuzi wa kufuta leseni ya kuhodhi ardhi katika eneo hilo la mradi bila kujali gharama alizowekeza.

Msingi wa madai hayo unatokana na ukiukwaji wa Mkataba wa Uwekezaji (BIT) uliyosainiwa kati ya Serikali na UK & Ireland ya Kaskazini mwaka 1994, unaohusisha wanahisa wenza wa Indiana Resources waliomiliki leseni hiyo.

Kwa mujibu wa Indiana, wanahisa waliishawishi Serikali kurejesha leseni yao lakini haikuwezekana, kutokana na marekebisho ya Sheria ya Madini mwaka 2017 yanayoelekeza kuzifuta.

Naye, Wakili Mkuu wa Serikali, Dk Boniphace Luhende amesema zuio hilo linahusisha uwezekano wa kutoshikiliwa ndege za Serikali mpaka utaratibu wa pingamizi utakapokamilika.

Chanzo: Mwananchi