Serikali yapunguza 50% ya ada za tozo za leseni za maudhui

0
51

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa amesema Serikali inakwenda kuondoa 50% ya ada za tozo mbalimbali za leseni kwenye marekebisho ya Kanuni za maudhui ya mtandaoni na maudhui ya utangazaji katika redio na televisheni yaliyofanywa hivi  karibuni ili kuzalisha ajira na vipato  wananchi.
 
“ Serikali imeamua kwa dhati kufanya marekebisho ya  kanuni hizi  kwa kuwashirikisha  wadau wake ambapo sasa  katika kipindi kifupi kijacho  tutashuhudia   maboresho yanaleta  matumaini na  mapinduzi makubwa   kwenye sekta na  wadau wategemee ongezeko la ajira na kuboreka  kwa vipato vyao kwa kiwango kikubwa,” amesisitiza Bashungwa

Ameongeza kuwa ada kwa Leseni za ‘simulcasting’ imeondolewa kabisa ambapo ameeleza kwamba hatua hiyo imefikiwa baada ya kuzingatia maoni ya wadau ya kuiomba Serikali tahfifu ya ada husika ili waweze kumudu kulipa bila faini au kulimbikiza madeni ambapo amesema watoa huduma wanatazamiwa kuongezeka kutokana na viwango vya ada kuwa rafiki.

Baadhi ya mambo muhimu katika Marekebisho ya Kanuni za Maudhui ya Utangazaji – Redio na Televisheni ni pamoja na kuongeza ukomo wa vituo vya usikivu kwa leseni za wilayani kutoka kimoja hadi vitatu (3) katika eneo ambamo redio au televisheni ipo ambapo ameeleza kuwa marekebisho haya yanatazamiwa kuongeza usikivu wa redio na Televisheni katika maeneo yenye  milima na mabonde.

Aidha, Kanuni ya 37 ya mwaka 2018 imerekebishwa kwa kufuta kanuni ndogo ya (2) iliyozuia kuungana na kituo kingine ili kutoa matangazo (hookup) bila kibali cha Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ambapo kwa sasa kituo kitatakiwa kinatoa taarifa tu kwa TCRA tofauti na awali.

Kwenye Kanuni ya 37(4) serikali imeondoa masharti ya mgeni kusindikizwa studio kwa lengo la kuondoa kabisa masharti yaliyotaka mgeni wa kituo chochote cha huduma ya maudhui kutoruhusiwa kutembelea kituo hicho mpaka awe ameongozana na Afisa wa Serikali au TCRA

Kwa upande wa  Kanuni za maudhui ya Mtandaoni, mambo muhimu yaliyofanyiwa marekebisho katika Kanuni hizo kuwa ni pamoja na kuondoa masharti kwa watoa huduma wa Internet Cafes (Kanuni ya 2 na 13), kuondoa masharti ya kuwa na leseni kutokaTCRA (Kanuni ya 3), kuondoa Leseni za ‘Simulcasting’ ambapo mtoa huduma wa maudhui ya mtandaoni kwa simulcasting hatalazimika kukata leseni nyingine wala kulipia ada tofauti anaporusha maudhui yaleyale anayorusha katika redio au televisheni asilia.

Pia, kuondoa wajibu kwa watoa huduma kutunga sera ya matumizi na kufunga vifaa vya kuchuja maudhui mabaya (kanuni ya 9), kuondoa zuio la ‘Simulcasting’ kwa redio za wilayani na mikoani na kuondoa zuio la matangazo ya Betting na michezo bingine ya kubahatisha.

Send this to a friend