Serikali yaruhusu usafirishaji wanyamapori hai nje ya nchi

0
73

Serikali imeruhusu usafirishaji wa wanyama pori  hai nje ya nchi waliokuwa wamesalia kwenye mazizi na mashamba ya ufugaji baada ya zuio la mwaka 2016.

Taarifa ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) imesema ruhusa hiyo ni kwa miezi sita kuanza Juni 6 hadi Desembe 5, mwaka huu.

Ili kufanikisha zoezi hilo, wafanyabiashara wenye wanyamapori waliosalia na ambao wamefanyiwa uhakiki wanatakiwa kuwasilisha nyaraka zote muhimu katika ofisi za utalii na huduma za biashara jijini Arusha karibu na ofisi za jeshi la zima moto, na Dar es salaam jengo la mpingo.

Aidha, taarifa hiyo imeeleza kuwa usafirishwaji wa Wanyamapori hao utafanyika kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Hata hivyo taarifa imesema wadau watakaoruhusiwa kusafirisha Wanyamapori ni wale wenye leseni ya biashara ya nyara (TDL) zilizohuishwa kwa mujibu wa sheria ya uhifadhi wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009.