Serikali imesema kwamba haina taarifa na haiwatambui watu waliohusika kuvunja vibanda vya wafanyabiashara wadogo na kuwajeruhi baadhi ya wafanyabiashara katika eneo Vingunguti jijini Dar es Salaam.
Katika tukio hilo lililotokea usiku wa kuamkia Septemba 23, 2021 mtu mmoja amedaiwa kupoteza maisha. Wakazi wa eneo hilo wamesema kwamba hawakupewa taarifa yoyote kuhusu uvunjaji huo ulioanza kutekelezwa saa 9 usiku.
Wafanyabiashara 45,000 Dar es Salaam wageuki Umachinga
“Nimevunjiwa kibanda changu, na kuna mwingine anauza vipodozi hapo kuvuka barabara, amepigwa sana, kajeruhiwa, yupo [Hospitali ya] Amana, kalazwa,” amesema Happiness James ambaye ni mamalishe kwenye eneo hilo.
Hamis Chogelo ambaye ni Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Miembeni amesema kwamba hakupewa taarifa kuhusu tukio hilo, na kwamba ilitakiwa ajulishwe, ili naye awajulishe wafanyabiashara waondoe mali zao kwa utaratibu.
Mchinga wapewa siku 7 waondoe biashara barabarani
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng’wilabuza Ludigija amesema hatambui tukio hilo la uvunjani wa vibanda kwa sababu sio agizo la serikali na kwamba watafanya uchunguzi ili kuwachukulia hatua wote waliohusika
“Kwa operesheni ambayo mmeisikia Vingunguti haijafanywa na halmashauri wala serikali, na mimi kama mkuu wa wilaya naendelea kufuatilia,” amesema Ludigija, huku akiongeza kuwa hana taarifa za mtu aliyeuawa katika tukio hilo, lakini ameahidi kufuatilia.
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla alitoa muda wa mwezi mmoja kwa wilaya zote kuandaa utaratibu wa kuwahamisha wafanyabiashara hao kwenda maeneo maalum ya kufanyia biashara zao.