
Serikali imeweka wazi msimamo wake kuhusu hali ya kisiasa nchini, ikisisitiza kuwa hakuna sheria yoyote iliyovunjwa katika utekelezaji wa majukumu yake kama taifa huru linalozingatia utawala wa sheria.
Akizungumza na wahariri jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, amesema serikali imekuwa wazi kuhusu masuala yote yanayohusu mwenendo wa kisiasa nchini. “Hatujavunja sheria yoyote ile na tumeendelea kuzingatia sheria.”
Kauli hiyo imekuja kufuatia sintofahamu iliyojitokeza miongoni mwa baadhi ya wanasiasa wa upinzani, baada Jeshi la Polisi kumshikilia Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Tundu Lissu, ambaye anakabiliwa na kesi ya uhaini.
Aidha, Serikali imeendelea kusisitiza kuwa itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria, na kwamba haki na taratibu zote za kisheria zitafuatwa ipasavyo kwa kila mwananchi, bila kujali nafasi yake ya kisiasa na kijamii.