Serikali yataja miradi mipya ya umeme inayofuata baada ya Stigler's Gorge

0
38

Rais Dk Magufuli amesema kuwa Serikali inatarajia kujenga mradi wa kuzalisha umeme katika mto Ruhudji utakaozalisha megawati 359, mradi wa Lumakali megawati 222, mradi wa kakono megawati 87, Rusumo megawati 80 na mingine itakayotumia nishati ya gesi, makaa ya mawe, jua, jotoardhi, upepo na urani.

Ameyasema hayo leo wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme katika mto Rufiji Mkoani Pwani ambao utakamilika Juni 2022 na kuzalisha megawati 2,115.

Katika hotuba yake, Mhe. Rais Magufuli ameipongeza Wizara ya Nishati kwa kusimamia utekelezaji mradi huo na ameeleza kuwa Serikali imechukua hatua za kujenga bwawa hilo ili kuongeza uzalishaji wa umeme nchini kutoka megawati 1,601 zinazozalishwa hivi sasa, hadi kufikia megawati 10,000 ifikapo mwaka 2025.

Amewataka wakandarasi wanaojenga mradi (Arab Contractors na Elsewedy Electric za Misri) kukamilisha mradi huo utakaogharimu shilingi za Kitanzania Trilioni 6.5 kabla ya Juni 2022 hasa ikizingatiwa hakuna tatizo la fedha ili Watanzania waanze kunufaika mapema.

Amependekeza bwana hilo liitwe Bwawa la Nyerere ikiwa ni kutambua na kuenzi maono ya Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere aliyetaka kujenga bwawa hilo wakati wa uongozi wake.

Send this to a friend