Serikali yataja sababu za sukari kupanda bei

0
43

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Stella Manyanya amesema kupanda kwa bei ya sukari huenda kunachangiwa na upungufu wa bidhaa hiyo sokoni, hivyo amewataka wananchi kutumia asali kama bidhaa mbadala.

Manyanya ameyasema hayo katika kikao kilichoitishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambacho pia kimehusisha wadau wa sukari nchi kikilenga kuangalia uwezekano wa kupunguza bei ya bidhaa hiyo wakati wa kuelekea kwenye mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

“Wananchi wapunguze matumizi ya sukari, kwanza hata kiafya sio nzuri sana, kama mtu asali haimdhuru basi ni bora akatumia asali,” amesema Manyanya.

Manyanya ameongeza kuwa sababu nyingine inayoweza kuwa imepelekea kupanda kwa bei ya sukari amesema kutokana na mlipuko wa virusi vya corona, nchi nyingi
zimesimamisha uzalishaji na pia mvua nyingi katika baadhi ya maeneo imesababisha uzalishaji kuwa mdogo.

“Mvua nyingi zinasababisha changamoto katika uzalishaji wa sukari, ile miwa ikiwa na maji mengi uzito wa sukari unapungua,” ameeleza kiongozi huyo.

Bidhaa hiyo ambayo kipindi cha nyuma waziri mkuu alitoa bei elekezi akitaka iuzwe shilingi 1,800 kwa kilo moja, katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam inauzwa kwa zaidi ya shilingi 3,000 kwa kilo moja.

Send this to a friend