Serikali imetangaza nafasi za ajira za walimu 6,949 wa Shule za Msingi na Sekondari zinazolenga kujaza nafasi wazi za watumishi waliokoma utumishi wao kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo vifo, kuacha kazi, kufukuzwa kwenye utumishi na kustaafu.
“Tumepata kibali cha ajira za walimu 6,949 pamoja na watumishi 2,726 wa kada ya afya. Hivyo, nachukua fursa hii kuutangazia umma kuwa taratibu za kuanza mchakato wa kuomba ajira hizo umekamilika na kwamba waombaji wote wenye nia ya kuomba, sasa wanaweza kufanya hivyo,” Waziri wa TAMISEMI, Ummy Mwalimu.
Alifafanua kuwa waombaji wanatakiwa kutuma maombi yao kwa njia ya mtandao kupitia kiunganishi ajira.tamisemi.go.tz kuanzia Mei 09 hadi 23 mwaka huu.
Hata hivyo, alieleza kuwa kwa upande wa watu wenye ulemavu hawatalazimika kutuma maombi yao kwa njia ya mtandao badala yake watatuma maombi yao yakiwa katika nakala ngumu.
Ummy almesisitiza kuwa kila mwombaji ni lazima awe Raia wa Tanzania mwenye umri usiozidi miaka 45, awe na namba ya kitambulisho cha Taifa, awe na vyeti kamili vya mafuzo ya fani aliyosomea na asiwe mwajiriwa wa Serikali au aliyewahi kuajiriwa na Serikali.