Serikali yatangaza oparesheni dhidi ya wanaosambaza maudhui ya kumdhalilisha Rais

0
148

Waziri wa Mambo ya Ndani, Innocent Bashungwa ameliagiza Jeshi la Polisi kupitia Mkuu wa Jeshi hilo, IGP Camillus Wambura, kuhakikisha linaweka mikakati madhubuti ya kuwasaka na kuwachukulia hatua wanaotengeneza na kusambaza maudhui ya kumdhalilisha Rais Samia Suluhu Hassan.

Akiwasilisha bungeni makadirio ya bajeti ya wizara kwa mwaka wa fedha 2025/26, Waziri Bashungwa amesema licha ya baadhi ya maudhui hayo kutengenezwa nje ya nchi, kuna Watanzania walioko ndani ambao wamekuwa wakiyapokea na kuyasambaza mitandaoni.

“Kazi nzuri ambayo Jeshi la Polisi linafanya kwa kushirikiana na TCRA [Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania] inapaswa kuongezwa nguvu maradufu ili kuhakikisha watu hawa wanashughulikiwa,” amesema Bashungwa.

Aidha, amesema Serikali haitofumbia macho kitendo cha watu wanaojiita wanaharakati kutoka nje ya nchi kuingia nchini kwa lengo la kuharibu amani iliyopo Tanzania.

Bashungwa amevitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuendelea kuimarisha usalama nchini ili Tanzania iendelee kuwa na amani na utulivu hususan ni wakati ambapo nchi inaelekea kwenye uchaguzi.

Send this to a friend