Serikali yatatua mgogoro kati ya mwekezaji na wachimbaji wadogo Mbeya

Waziri wa Madini, Anthony Mavunde ameeleza kuwa wananchi wa Kata ya Ifumbo Wilayani Chunya watapewa leseni 2 kati ya 14 za uchimbaji madini zinazomilikiwa na Kampuni ya G & I katika bonde la Mto Zira na kutambulika rasmi kama wachimbaji halali ili wafanye shughuli za uchimbaji bila usumbufu ikiwa ni hatua ya utatuzi wa mgogoro baina ya wananchi hao na mwekezaji.
Amesema hayo Aprili 28, 2025 wakati akizungumza katika Mkutano wa hadhara na wananchi wa Kata na Kijiji cha Ifumbo Wilayani Chunya akiwa ameambatana na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Khamis Hamza Chilo.
“Tunamshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo yake kushughulikia haya mambo kwa uharaka sana na tuko hapa kwa utekelezaji wa maelekezo yake,” amesema.
Ameongeza kuwa “Baada ya kusitisha shughuli za uchimbaji madini katika bonde hilo mwishoni mwa mwezi Desemba 2024 niliunda Kamati ya Wataalam ya kutathmini athari za mazingira yaliyotokana na shughuli za uchimbaji madini katika mto Zira.
Kwa kuwa wananchi wa hapa shughuli zenu zinategemea Mto Zira, nimemwelekeza mwekezaji ili aendelee kudumisha ujirani mwema, tumekubaliana katika leseni 14 anazomiliki, atoe leseni 2 kwa ajili ya wananchi wa Ifumbo na Lupa Market ikiwa ni leseni moja kwa kila kijiji, ambako atafanya tathmini ya mazingira kabla hajakabidhi kwa serikali ya kijiji, tathmini hii ni kwa leseni 7 zilizopo Ifumbo kwa kuwa 7 zilizopo Lupa Market zimeshafanyiwa tathmini.”
Amesema Kampuni ya G & I ihakikishe kuwa mazingira yanarejershwa kama yalivyokuwa awali kabla uchimbaji haujaanza (restoration); iweke mipaka ya leseni zao zinapoishia; Uchimbaji wa eneo la ifumbo uendelee kusimama mpaka utaratibu wa kimazingira utakapokamilika.
Desemba 30, 2024, Waziri Mavunde alitangaza kusitisha shughuli za uchimbaji madini katika bonde la mto Zira na kuahidi kuunda Kamati Maalum itakayofanya tathmini ya uharibifu wa mazingira uliotokana na shughuli za uchimbaji madini na baada ya kamati hiyo kukamilisha kazi yake ataleta mrejesho.