Serikali yatenga bilioni 114 ukarabati barabara za mikoa ya Kusini zilizoathiriwa na El Nino

0
8

Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 114 kukarabati barabara za mikoa ya Kusini zilizoharibiwa na mvua za El Nino, huku akiagiza taa za kutosha kuwekwa kwenye barabara kuu kuelekea mikoa hiyo.

Akizungumza katika maeneo tofauti wakati wa ziara yake mkoani Lindi, Ulega amesema kiasi hicho cha fedha kilichotengwa kwa Mkoa wa Lindi ndiyo kikubwa zaidi kutengwa kuliko mkoa mwingine wowote hapa nchini.

“Ndugu zangu wa Lindi, nimekuja kukagua barabara zetu baada ya matatizo ya mvua za El Nino na hiki kimbunga cha Hidaya. Rais ameniagiza nije huku kuangalia hali na kuwapa pole kwa changamoto mnazopitia.

“Kwa mapenzi yake makubwa kwenu na kwa Watanzania kwa ujumla wake, Rais Samia ameagiza tutumie zaidi ya shilingi bilioni 114 kwa ajili ya kurekebisha barabara na madaraja yaliyoharibiwa na kutengengeza njia za kuchepusha,” amesema Ulega wakati akiwa eneo la Somanga.

Mvua za El Nino zilizonyesha nchini mwishoni mwa mwaka jana na kufuatia msimu wa mvua za masika, zilisababisha uharibifu mkubwa wa miundombinu katika maeneo tofauti nchini, ingawa mikoa ya Kusini iliathirika zaidi.

Katika hatua nyingine, Ulega ameagiza Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuanza kuweka taa katika barabara kuu inayoelekea mikoa ya Kusini ili kukuza shughuli za kiuchumi katika maeneo inakopita.